WATOA HUDUMA HAKIKINI KADI ZA WANACHAMA WA NHIF KUEPUKA UDANGANYIFU

WATOA HUDUMA HAKIKINI KADI ZA WANACHAMA WA NHIF KUEPUKA UDANGANYIFU Feb 21, 2022

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umewataka Watoa huduma nchini hususan wa Maduka ya Dawa, kujiridhisha na taarifa za wanachama wanaokwenda kuchukua dawa katika vituo vyao.

Rai hiyo imetolewa Jijini Mbeya na Meneja wa NHIF Kitengo cha Kupambana na Udanganyifu Dkt. Rose Ntundu kwenye kikao cha Baraza la Wafanyakazi, ambapo amesema watoa huduma za matibabu wengi wamekuwa wakitoa dawa kwa baadhi ya wanachama bila kuhakikisha endapo ni wanachama halisi kupitia kadi zao.

“Pamoja na kwamba tunao Mfumo wa utoaji dawa - Phamacy Portal ambao huwekwa taarifa za mwanachama kutoka Kituo cha matibabu alichotibiwa na kukosa dawa alizoandikiwa lakini ni lazima pia wahakikishe wanachama hao wanapokwenda kuchukua dawa wawe na kadi zao na kuzihakiki kama ndio wahusuka,” alisema.

Alisema kuwa suala la kulinda uhai wa Mfuko sio la NHIF peke yake bali ni jukumu la kila mdau wa Mfuko wakiwemo Watoa huduma, wanachama na wananchi kwa ujumla. “Tukishirikiana kwa pamoja kutoa taarifa za udanganyifu zitasaidia sana kulinda uhai na kukomesha vitendo hivi,” alisema Dkt., Ntundu.

Alitumia mwanya huo kuwaomba wananchi wote kushirikiana na Mfuko kutoa taarifa zenye viashiria vya udanganyifu kupitia namba 0800 111163 ambayo ni bure na taarifa hizi ni za siri na mtoa taarifa analindwa.

Dkt. Ntundu amewaomba wananchi ambao wako nje ya Mfumo wa huduma za bima ya afya kujiunga na NHIF kwa utaratibu sahihi kabla ya kuugua ili kuepukana na vishawishi vya kuingia kwenye udanganyifu wakati wanapopatwa na maradhi.
“Tunapombaini mtu amefanya udanganyifu hatua kali za kisheria zinachukuliwa hivyo ili kuepukana na hili ni vyema kila mwananchi akajiunga na NHIF ili kuwa na uhakika wa huduma za matibababu wakati wote na popote nchini.

Mwisho.