WAZIRI MKUU AZINDUA FAO LA USHIRIKA AFYA LA NHIF

WAZIRI MKUU AZINDUA FAO LA USHIRIKA AFYA LA NHIF Jul 17, 2018

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua fao la Ushirika Afya ambalo linawalenga wananchi wanaojishughulisha na kilimo kupitia ushirika.

Amezindua fao hilo jana (Jumatatu, Julai 16, 2018) kwenye mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ulowa katika kijiji cha Kangeme, kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Shinyanga.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi 20 kwa niaba ya wanachama 259 ambao wamejiunga na mpango huo. Wanachama hao wanatoka katika vyama mbalimbali vya ushirika kwenye Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.

Amesema katika kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za afya katika hospitali yoyote ile nchini, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, wameamua kuzindua mpango wa Ushirika Afya, ambao unahusisha wakulima walio katika vyama vya ushirika.

“Gharama ya kujiunga na fao hili kwa mwaka ni sh. 76,000 kwa mtu mmoja na sh. 50,400 kwa mtoto mmoja lakini unakuwa na uhakika wa kutibiwa katika hospitali yoyote ile hapa nchini,” amesema.

Amesema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Tanzania kuna vyama vya ushirika 10,522 vyenye wanachama 2,234,000 ambapo asilimia 35 ya wanaushirika huwa wanapata magonjwa ya dharura na wanakuwa hawana namna ya kupata fedha kwa haraka.

“Tunatambua wote kuwa fedha ya mkulima ni ya msimu, lakini mkulima ukiwa na kadi ya bima ya afya, utapata matibabu kokote kule hata kama huna fedha taslimu,” amesema.Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza kijana aliyebuni mpango huo ambaye anatoka Taasisi ya Ukuzaji wa Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Mwombeki Baregu.

“Huyu kijana si mwajiriwa wa NHIF, wala siyo mtumishi Serikalini, lakini kwa sababu ya uzalendo, alikuja na huu mfumo akauelezea na kuonesha manufaa yake kwa wananchi wa kawaida, na kwa sababu Serikali yenu ni sikivu, tukaufanyia kazi na leo ninauzindua,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga amesema kuna vyama vya ushirika takribani 10,000 ambavyo vina wanachama zaidi ya milioni 2.5 wanaojishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo pamba, korosho, tumbaku, chai na kahawa."Lengo letu ni kuwafikia wanachama hawa pamoja na familia zao ili kuwawezesha wapate huduma katika kipindi cha mwaka mmoja tangu siku alipochangia.

"Kupitia utaratibu huu, mwanachama atapata huduma za uchunguzi na matibabu katika vituo zaidi ya 6,000 vilivyosajiliwa na mfuko wetu nchi nzima," amesema.

Ameongeza “Kupitia mpango huu wa ushirika afya, mwanachama atapata huduma za vipimo na matibabu mpaka ngazi ya Taifa kulingana na ushauri wa wataalam. Mfuko kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika, itaendelea kutoa elimu kwa wanachama wa ushirika kwa lengo la kuongeza uelewa wa mpango huu kwa walengwa.”

Amesema NHIF imeufanyia maboresho mpango huo ambapo kwa sasa wameanzisha vifurushi mbalimbali ambapo mwanachama ataweza kuchagua kulingana na uwezo wake na ukubwa na hali ya familia yake.

“Vifurushi hivyo vinaanzia kwa mwanachama aliye peke yake, aliye na mwenza, aliye na mwenza na mtoto mmoja, wawili mpaka wanne. Kwa mwanachama asiye na mwenza lakini ana familia, mpango huu umeweka utaratibu wake,” amefafanua.

Akitoa shukrani kwa Waziri Mkuu, Spika Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Mama Anne Makinda amesema uzinduzi uliofanyika jana umewakilisha kuzinduliwa kwa fao hilo kwenye mikoa yote nchini.

Amesema wana mpango wa kwenda kwenye mikoa yote inayozalisha mazao makuu matano ya kimkakatii ambayo ni chai, kahawa, pamba, tumbaku na korosho ili waweze kuwafikia wananchi wengi kwa urahisi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi kadi ya bima ya afya mmoja wa wakulima waliopo kwenye Ushirika huo ambapo wanachama 120 wamepatiwa kadi hizo na wanachama 200 wameshajaza fomu za kijiunga

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe mfano wa kadi ya bima ya afya kwa matibabu kwa vyama vya Ushirika wilayani Ushetu

Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa akimkabidhi kadi ya bima ya afya ya Ushirika Waziri Ummy Mwalimu

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bernad Konga akizungumzia Fao hilo ambalo litawanufaisha wakulima wa mazao waliopo kwenye vyama vya msingi.

Wananchi wa kata ya Ulowa wakifuatilia uzinduzi huo.