Wekezeni Katika Afya Mpunguze Matumizi ya Pesa Katika Anasa- RC Byakanwa

Wekezeni Katika Afya Mpunguze Matumizi ya Pesa Katika Anasa- RC Byakanwa Mar 12, 2020

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amewataka wananchi kujiwekea utaratibu wa kujikatia bima ya afya na kuacha kutumia pesa nyingi katika mambo ya anasa na kusahau kuhusu afya zao

Mhe. Byakanwa amesema hayo leo 19.12.2019 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na vifurushi vya bima ya afya Mkoani Mtwara.

Mhe. Byakanwa amesema kuwa umekuwa ni utaratibu kwa watanzania wengi kupeleka fedha nyingi katika vyama vya kufa na kuzikana badala ya kuwekeza fedha hizo katika afya zao.

“Ni lazima watanzania tubadilike, afya ndio kila kitu, watanzania tumekuwa wachangiaji wakubwa kwenye mambo ya anasa na kusahau kuwa afya ndio msingi wa mambo hayo yote, NHIF wamepunguza gharama kutoka Milioni Moja na Laki tano za hapo awali na sasa unalipa laki moja na tisini ta mbili tu kwa mwaka mzima kwa mtu mmoja, tujiunge tuwe na uhakika wa matibabu”-Alisema Byakanwa.

Aidha, Byakanwa alisema kuwa Mpango huu wa Vifurushi vya Bima ya Afya ni msingi wa kujenga taifa lenye uwezo wa kuzalisha mali, taifa lilio tayari kwenda katika uchumi wa kati, taifa lililo tayari kujenga uchumi wa viwanda na taifa lenye watu wenye afya njema.

Akioongea wakati wa uzinduzi huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mhe. Anne Makinda alisisitiza kuwa taifa lolote lenye kuhitaji maendeleo lazima liwe na wananchi wenye afya hivyo watanzania hawana budi kuweka utaratibu wa kukata Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa matibabu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Evod Mmanda aliwapongeza NHIF kwa kuja na mpango huu wa Vifurushi vya Bima ya Afya vitakavyowezesha idadi kubwa ya watanzania kuwa na Bima ya Afya.

Wakati huohuo Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga alisema kuwa waliamua kubuni mpango wa vifurushi ili kuhakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma ya Bima ya Afya na anakuwa na uhakika wa matibabu.

Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Mhe. Abdallah Chikota aliishukuru NHIF kuja na mpango huu kwani bunge limekuwa liibana serikali kwa muda mrefu kuhakikisha wanakuja na mpango ambao utawajumuisha watanzania wengi zaidi.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umezindua vifurushi vipya vya Bima ya Afya vilivyopewa majina ya NAJALI AFYA, TIMIZA AFYA na WEKEZA AFYA vyenye lengo la kujumuisha watanzania wengi zaidi hasa walio katika ajira zisizo rasmi.