Mpango wa Dunduliza

Katika kutimiza dhamira ya Serikali ya kuwawezesha Watanzania kuwa kwenye mfumo bima ya afya, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeanzisha mpango maalumu wa malipo ya michango kwa awamu ujulikanao kama Dunduliza.

Mpango huu wa Dunduliza unawawezesha wananchi wenye vipato tofauti tofauti kudunduliza michango yao kidogo kidogo kadiri wanavyopata kupitia akaunti maalumu ya Benki hadi pale kiwango cha mchango kitakapokamilika. Mwanachama atapatiwa kitambulisho cha NHIF atakachotumia kupata huduma za matibabu kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyoainishwa.

MAELEZO MUHIMU YA KUZINGATIA

- Utaratibu huu kwa sasa unatumika kwa wanachama wanaojiunga kupitia vifurushi vya NAJALI AFYA, WEKEZA AFYA na TIMIZA AFYA. Mfuko utaendelea kuboresha mfumo ili kuweza kujumuisha makundi mengine,

- Mwanachama atachangia kidogo kidogo kupitia kibubu cha benki ya NMB na anapokamilisha kiasi anachotakiwa kulipa kulingana na kifurushi alichochagua, mchango wake utawasilishwa kwenye Mfuko kupitia utaratibu wa malipo wa Serikali (GePG),

- Ili kujisajili na mpango wa dunduliza mwanachama anatakiwa kufika katika tawi lolote la Benki ya NMB lililo karibu naye au kujisajili kwa njia ya simu kwa kutumia namba *150*68# na kuchagua huduma ya kibubu kisha kufuata maelekezo hadi mwisho.

- Kupitia mpango huu, mwananchi ana fursa ya kulipia kwa awamu kifurushi alichokichagua kuanzia miezi miwili hadi miezi kumi na mbili,

- Wanachama wa vifurushi vya bima ya afya watakaojiunga kupitia utaratibu huu hawatakuwa na muda wa kusubiri mara wanapokamilisha kiwango cha mchango husika,

- Wanachama ambao watajumuisha wategemezi wanatakiwa kuwasilisha viambatisho vya uhusiano kupitia tovuti ya mfuko www.nhif.or.tz au kufika katika ofisi za Mfuko na kisha kuruhusiwa kudunduliza.

VIGEZO NA MASHARTI YA UTARATIBU WA KUDUNDULIZA

- Kuweka fedha kwa utaratibu wa kudunduliza mpaka zitakapofikia kiwango kinachohitajika;

- Atapatiwa kadi ya matibabu ya NHIF mara baada ya kukamilisha kwa kiwango cha mchango kinachohitajika;

- Vigezo na masharti kwa kundi la Vifurushi vitazingatiwa