Wasifu wa NHIF

Dira

Kuwa bima bora ya afya inayoongoza Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Dhamira

Kujikita katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma na kutoa bima bora ya afya kwa wanufaika.

Maadili

Kujenga imani ya wanachama katika uadilifu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Katika utendaji wote, Mfuko utahimiza utamaduni unaoakisi maadili yafuatayo:-

i. Uadilifu
ii. Uwajibikaji
iii. Ubunifu
iv. Heshima
v. Uharaka
vi. Hadhari

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni Taasisi ya Bima ya Afya iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Bima ya Afya, Sura namba 395 kwa lengo kuu la kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya kwa watu. Ni taasisi ya Serikali inayofanya kazi chini ya Wizara ya Afya. Usimamizi wa Mfuko ni wa Bodi ya Wakurugenzi huku shughuli zake za kila siku zikisimamiwa na Mkurugenzi Mkuu.

Pamoja na utaratibu wa uandikishaji watumishi wa umma, Mfuko umeongeza wigo wake na kujumuisha vikundi vingine kama Madiwani, kampuni binafsi, taasisi za elimu, watu binafsi, watoto chini ya umri wa miaka 21, wakulima katika vyama vya ushirika pamoja na vikundi vilivyosajiliwa kama machinga na vikundi vya bodaboda. Mfuko pia unasimamia Mpango wa Bima ya Afya ya Bunge na unahudumia Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Udhibitisho wa ISO 9001:2015

Mfuko wa Kitaifa wa Bima ya Afya umethibitishwa na viwango vya ISO 9001:2015 tangu 2018 ili kukubaliana na manufaa ya mfumo wa usimamizi wa ubora ambao huongeza ufanisi na kupunguza hasara pamoja na kuongeza kuridhika kwa wateja.

Majukumu ya Msingi ya Mfuko

Majukumu ya msingi ya Mfuko ni:-

• Kusajili wanachama na kutoa vitambulisho;

• Kukusanya michango;

• Kusajili watoa huduma za afya kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wanachama;

• Kulipa madai ya watoa huduma za afya;

• Kuwekeza fedha za ziada zilizokusanywa ili kupata mapato;

• Kufanya tathmini ya uhai wa Mfuko;

• Kutoa elimu ya bima ya afya kwa umma.

Michango

Kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya, wafanyakazi katika sekta ya umma wanalazimika kujiandikisha na kuchangia Mfuko jumla ya asilimia sita (6%) ya mishahara yao ya msingi ya mwezi ambayo inagawanywa kwa usawa kati ya mwajiri na mwajiriwa. Hata hivyo, Mfuko umeweka utaratibu tofauti wa uchangiaji kwa vikundi vingine vinavyojiunga na Mfuko kwa hiari.

Wanufaika

Wanufaika wa NHIF katika mpangilio wa familia ni pamoja na mshiriki anayechangia, mwenzi wake na hadi wategemezi wanne wanaotambulika kisheria. Hadi kufikia Juni 2024, jumla ya wanachama wa NHIF walikuwa wanufaika 5,026,069 ambayo ni sawa na 8% ya Watanzania wote.

Makundi ya Wanachama wa NHIF

Wanachama wa Mfuko wameainishwa kama ifuatavyo:-

• Wafanyakazi wa Umma

• Watumishi wa taasisi binafsi

• Wastaafu wa sekta ya UMMA

• Wanafunzi

• Watoto walio chini ya umri wa miaka 21

• Wakulima katika Vyama vya Ushirika vya Msingi

• Wanachama wa vikundi vya kijamii vilivyopangwa mfano Machinga, Bodaboda, Madereva n.k.

• Wanachama binafsi

• Mpango wa Bima ya Afya ya Bunge kwa Wabunge.

• Madiwani

Kitita cha Mafao

1. Kujiandikisha na kumwona daktari.

2. Vipimo.

3. Dawa na vitendanishi

4. Huduma za kulazwa

5. Upasuaji mdogo, mkubwa na wa kitaalamu.

6. Huduma za afya ya meno na kinywa

7. Matibabu ya macho.

8. Huduma za mazoezi ya viungo (physiotherapy)

9. Miwani ya kusomea kwa mwanachama mchangiaji

10. Vifaa saidizi (Medical/ Orthopedic appliances)

Huduma Zinazohitaji Vibali Maalum

Ili kupata huduma za matibabu zinazohitaji vibali maalumu mwanachama hatalazimika kwenda makao makuu kufuata kibali kama hapo awali. Vibali vinatolewa katika ofisi za NHIF za mikoa na katika baadhi ya vituo vya matibabu vilivyowezeshwa.

Huduma hizi ni pamoja na:-1.Vipimo vya MRI na CT-Scan

2.Vifaa tiba saidizi (Orthopaedic Appliances)

3.Huduma ya nyenzo saidizi (Implants)

4.Huduma za miwani ya kusomea kwa mwanachama mchangiaji.

5.Huduma za kusafisha damu (Haemodialysis)

6.Dawa za kuongeza uzalishaji wa damu (Erytrhropoietin)

7.Dawa za Saratani (Chemotherapy)

8.Huduma kwa waliopandikizwa Figo (Immuno-suppressants/ Immuno-stimulants)

9.Huduma za mionzi (Radiation Therapy)

10.Baadhi ya dawa

11.Huduma za IOCT,EMG needle,Albumin infusion na Polypylene Mesh12.Huduma za upasuaji wa Moyo

Mwanachama anayehitaji kupata baadhi ya huduma za vibali maalum kwa mara ya kwanza atafunguliwa faili katika ofisi iliyo karibu nae. Atakapohitaji kibali hicho hicho kwa mara ya pili atahudumiwa huko huko hospitali.NHIF pia hurahisisha utoaji wa huduma ambazo kwa kawaida huwa nje ya kitika cha mafao, chini ya makubaliano maalum kulingana na hitaji la mwajiri kupitia mipango ya Huduma za Ziada.

Vitengo na Mtandao wa Vifaa vya Afya vilivyoidhinishwa

Mfuko unafanya uhakiki wa vituo ambavyo vimesajiliwa kikamilifu na Wizara ya Afya ili kutoa huduma kwa walengwa. Vituo hivi vya afya vimegawanyika katika makundi matatu ambayo ni Serikali, Mashirika ya Dini na vituo Binafsi. Hivi sasa Mfuko umesajili vituo zaidi ya 8,051 vyenye viwango tofautiili kuwahudumia wanufaika wa Mfuko. Vituo hivyo ni kama ifuatavyo:-

• Hospitali za Rufaa za Taifa,

• Hospitali za Rufaa za Kanda,

• Hospitali za Rufaa za Mkoa,

• Hospitali za Wilaya,

• Vituo vya Uchunguzi

• Kliniki na Kliniki Maalumu,

• Vituo vya Afya,

• Zahanati, na

• Maduka ya dawa

Mtandao wa Ofisi za Mikoa za NHIF

NHIF imeanzisha ofisi katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar ili kusogeza huduma zake karibu na wanachama na wananchi kwa ujumla.