Umoja Afya

Umoja Afya ni nini?

Ni utaratibu wa bima ya afya unaowalenga wajasiriamali waliojiunga katika makundi mbalimbali yanayotambuliwa na mamlaka za Serikali. Utaratibu huu unawawezesha wanaumoja wa makundi hayo kuchangia huduma za afya kwa umoja wao na kunufaika na bima ya afya kupitia mtandao mpana wa vituo zaidi ya 7,700 vilivyosajliwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhudumia wanachama wake ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Makundi hayo ni kama Umoja wa Babalishe na Mamalishe, Umoja wa Wafanyabiashara Sokoni, Umoja wa Wauza Samaki, Umoja wa Wauza Maziwa, Umoja wa Wakata Miwa, Umoja wa Wachuma Chai, Umoja wa Wakata Mkonge, na Umoja wa Wachimbaji Wadogo wa Madini.

Wanufaika ni akina nani?

Wanufaika ni wanachama wa makundi hayo, wenza wao na watoto wasiozidi wanne wa kuzaa au kuasili wenye umri chini ya miaka 18.

Madhumuni ya Mpango wa Umoja Afya

  • Kutoa fursa kwa wananchi walio katika makundi mbalimbali ya shughuli za kiuchumi kunufaika na huduma za bima ya afya zinazotolewa na Mfuko;
  • Kulinda mitaji ya wanachama kwa kuwapa uhakika wa matibabu kupitia kadi ya bima ya afya inayowawezesha kupata huduma za matibabu.

Jinsi ya kujisajili na mambo muhimu ya kuzingatia

  • Mwanachama anatakiwa kujaza fomu ya kujiunga (inapatikana katika ofisi za Mfuko au tovuti ya Mfuko www.nhif.or.tz ) kupitia Uongozi wa Umoja/kikundi husika.
  • Kikundi au Umoja uwe umetambuliwa na mamlaka za Serikali.
  • Utaratibu wa Umoja Afya utahusisha usajili wa kundi zima na siyo mwanachama mmoja mmoja na fomu za uanachama, viambatanisho na taarifa zote muhimu za wategemezi zitawasilishwa kwenye Mfuko kupitia Chama au Umoja wao.
  • Mchango wa kila mwanachama ni Shilingi 100,000 kwa mwaka. Aidha, mwanachama atamlipia mwenza Shilingi 100,000 na mtoto Shilingi 50,400 pindi atakapotaka kuwaunganisha.
  • Michango ya wanachama wote italipwa kwa mkupuo kupitia kwa chama au umoja husika.
  • Mwanachama anatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa au namba ya kitambulisho cha uraia wakati wa usajili.
  • Mwanachama atapata kitambulisho cha matibabu kwa kuzingatia vigezo na masharti ya mpango wa UMOJA AFYA.

Kwa maelezo zaidi wasiliana na ofisi ya Mfuko iliyokaribu na wewe au wasiliana nasi kupitia simu ya huduma kwa wateja bila malipo 0800 110063.